Maisha ni safari na wala kakuna binadamu anayejua mwisho wa safari yake hapa duniani. Maisha ni fumbo kwani hakuna binadamu mwenye uhakika wa maisha yake ya kesho, tuishi vizuri leo kwani kesho siyo yetu. Maisha ni mtihani ni lazima kutafuta majibu sahihi ya mtihani wa maisha yetu. Maisha ni uchanguzi kila siku tunachagua hatima ya maisha yetu.
Maisha ni fursa ambayo Mungu kamjalia kila binadamu kusudi tufanye yale tuliyokusudiwa kuyafanya maishani mwetu, tuitumie fursa ya maisha vizuri. Maisha ni zawadi ni vema nasi turudishe zawadi ya shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya maisha aliyotujalia, tuitunze zawadi ya maisha.
Maisha ni dira yetu tukiyaongoza vema, maisha yetu yatatuongoza katika njia sahihi ya kufikia lengo la maisha yetu. Maisha ni mfano wa kilima kadiri mtu anavyofanikiwa ndivyo anavyozidi kupanda juu, lakini kumbuka, maisha ni kupanda na kushuka. Maisha ni kama mfano wa daraja la kutuvusha nga’mbo ya pili, maisha yetu yatasaidia kuimarisha au kulibomoa daraja la kutuvusha ng’ambo ya pili.
Maisha ni mfano wa gari unaweza kuliongoza na kulipeleka kokote unakotaka liende, hata porini litakwenda, wewe ni dereva wa maisha yako. Maisha ni mfano wa barabara yenye kona nyingi ni vigumu kuona kilichopo mbele yetu Mungu anaona na anajua mwisho wetu. Mitihani yote ya maisha ya duniani tunaweza kufaulu vizuri, lakini mtihani wa mwisho wa maisha yetu ya duniani ni fumbo lisilofahamika. Maisha ni kitendawili na jibu lake analo Mungu peke yake.
"Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi Mungu; unifundishe nifuate unayotaka. Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha, kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu; nakutegemea wewe kila siku." Zaburi 25:4-5 "Nani anayetambua uzito wa hasira yako? Nani anayejali matokeo ya ghadhabu yako? Utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima." Zaburi 90:11-12