Mwanangu, huu ni moyo wangu unaokupenda, hakuna moyo mwingine uliojaa mapendo kama moyo wangu. Usiache kuutafakari moyo wangu mtakatifu. Hakuna moyo mwingine utakaokupenda, kama moyo wangu unavyokupenda. Huwezi kujua ni kwa jinsi gani ninakupenda mpaka utakapoweza kunipenda kwa moyo wako wote.
Moyo wangu umejaa huruma nyingi kwa wakosefu wanaonikimbilia kwa moyo wa majuto. Moyo wangu haujawahi kumkataa mkosefu yeyote anayetubu na kunipenda. Usiache kuukimbilia moyo wangu kila unapoanguka mwanangu. Huruma yangu ipo kwa ajili yako upate kuhurumiwa na kusamehewa makosa yako.
Moyo wangu umepata maumivu makali na bado naendelea kuteseka moyoni mwangu kila unapokataa kutubu dhambi zako na kuendelea kutenda dhambi. Ni moyo wangu tu unaoweza kukuvumilia katika hali yako ya dhambi na kukupokea tena kila unapotubu. Jitahidi kunipenda mwanangu upunguze maumivu ya moyo wangu, ninakupenda lakini nitakupenda zaidi ukitubu dhambi zako na kuambatana nami.
"Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda mlimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Hata akimpata kumwona, amin, nawaambia, amfurahia huyo zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea. Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee." (Mathayo 18:12-14)